Page Nav

HIDE

Breaking News:

latest

DUNIA YA WALIMWENGU (1)

  DUNIA YA WALIMWENGU (1) “Mume wangu! Naomba unisamehe!” “Nikusamehe! Mara ngapi? Nahisi hunijui! Sasa subiri.” “Mume wangu naomba uni...


 DUNIA YA WALIMWENGU (1)

“Mume wangu! Naomba unisamehe!”
“Nikusamehe! Mara ngapi? Nahisi hunijui! Sasa subiri.”
“Mume wangu naomba unisamehe! Sitorudia tena!”
“Eti hutorudia! Unanifanya mimi mjinga! Leo nataka nikuonyeshee, utajua kwa nini Mungu alianza kumuumba Adamu kabla ya Hawa.”
Zilikuwa ni kelele kutoka katika nyumba moja chakavu iliyokuwa katika Mtaa wa Tandale kwa Tumbo jijini Dar es Salaam. Watu waliokuwa wakipita nje ya nyumba hiyo, walisimama na kusikiliza kile kilichokuwa kikiendelea.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza, kila siku kulikuwa na fujo ndani ya nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi watu wawili tu, Godwin Mapoto na mwanamke mrembo aliyewahi kutikisa kutokana na urembo wake, Winfrida Michael.
Kelele zile ziliendelea kuwakusanya watu wengi nje ya nyumba hiyo. Wale waliokuwa ndani ya nyumba zao, wakatoka na kwenda kusimama karibu kabisa na nyumba hiyo.
Hakukuwa na mtu aliyediriki kuingia ndani kugombelezea kwani walimfahamu Mapoto, japokuwa alionekana kuwa mwanaume dhaifu, mwenye mwili mwembamba lakini alivuma kutokana na ubabe wake mtaani hapo.
Alikuwa mwanaume wa fujo, aliyetikisa kuanzia Kwa Tumbo, Kwa Mtogole, Yemen mpaka Mwananyamala kwa Manjunju. Watu wengi walikuwa wakimuogopa, jina lake lilikuwa likivuma sehemu kubwa kuanzia Tandale, Mwananyamala mpaka Magomeni Kondoa.
Alikuwa mbabe wa mtaa kiasi kwamba watu walihisi kwamba asingekuja kuwa na mwanamke mrembo kutokana na ubabe wake, lakini kitu kilichowashangaza ni kwamba alifanikiwa kumnasa msichana aliyekuwa na sura nzuri, ya kipole, umbo matata, Winfrida Michael, msichana aliyekuwa akikubalika katika Chuo cha St. Joseph alipokuwa akisomea biashara.
Chuoni hapo, Winfrida alitingisha kwa uzuri, kila mwanaume alikuwa akimzungumzia yeye, alipokuwa akitembea, watu walimfananisha na twiga huku macho yake yakiwa na mvuto mithili ya mwanamke aliyekula kungu.
Hakuwa msichana mwepesi, alikuwa mgumu, wanaume walimfuata na kumtaka kimapenzi lakini Winfrida hakukubaliana nao hata kidogo. Kila walipokuwa wakizungumza naye, alionyesha tabasamu kubwa kiasi kwamba liliwapa matumaini wanaume wengi lakini jibu lake halikufanana na tabasamu alilokuwa akilitoa usoni mwake.
“Nimekuelewa,” alisema Winfrida.
“Sawa. Kwa hiyo?” aliuliza mwanaume mmoja, kama walivyokuwa wengine, na yeye alimfuata msichana huyo kwa lengo la kumtaka kimapenzi.
“Kwa hiyo nini Ibrahim? Nimekwishakwambia kwamba sikutaki! Kwa nini hutaki kusikia?” aliuliza Winfrida huku akionekana kuchukizwa na uwepo wa mwanaume huyo mbele yake.
“Winny! Ninakupenda sana. Wewe ni mwanamke wa ajabu sana mbele ya macho yangu, ni mwanamke mzuri sana. Nakuomba uwe nami, nakuahidi kwamba kamwe sitokuumiza, ninaapa kwa viapo vyote, kamwe sitokuumiza,” alisema mwanaume huyo, kwa kumwangalia tu, macho yake yalionyesha kumaanisha alichokuwa akikizungumza lakini kwa msichana kama Winfrida, ilikuwa ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa.
“Haiwezekani!”
Huyo hakuwa mwanaume wa kwanza kumfuata, wengi walifuata. Wengine walimwendea na gari kwa kuhisi kwamba msichana huyo angenasa katika mitego yao lakini waligonga mwamba, hakutaka kumuelewa mtu yeyote yule kiasi kwamba wanaume wengi wakajiuliza juu ya kitu alichokuwa akikihitaji msichana huyo.
“Labda gari?” alisema jamaa mmoja.
“Haiwezekani! Godwin alimfuata akiwa na gari!”
“Ikawaje?”
“Akapigwa cha mbavu!”
“Mh! Labda mkwanja!”
“Hata nao hauwezekani! Idris alimfuata akiwa na mkwanja wa kutosha, akamtamanisha lakini wapi! Labda tujaribu kuwa watumishi wa Mungu,” alisema jamaa mwingine.
Walikuwa wakizungumza mambo mengi kuhusu Winfrida, walianzisha mbinu nyingi za kumpata msichana huyo lakini hakukuwa na mtu aliyekubaliwa kitu kilichoendelea kuwaumiza mioyo yao.
Baada ya kumaliza mwaka wa kwanza, tena huku Winfrida akiwa kwenye chati kubwa machoni mwa wanaume wengi, akakutana na Godwin maeneo ya Makumbusho, mahali ambapo mwanaume huyo alipokuwa akifanya kazi ya kupiga debe.
Macho ya Winfrida yalipotua kwa Godwin akashtuka, mapigo yake ya moyo yalimuenda mbio, hakuamini kama siku hiyo angekutana na mwanaume kama huyo.
Alimvutia! Mwili wake uliojazia ambao ulionekana vilivyo ulimchanganya msichana huyo kiasi kwamba akabaki akimkodolea macho tu kiasi cha kumshangaza Happiness, rafiki yake aliyekuwa naye pembeni.
“Dada mnakwenda? Dada vipi hapo?” aliuliza Godwin huku akimwangalia Winfrida na Happiness, hakutaka kuridhika, akawafuata na kuwashika mkono na kuwavutia kwake kama walivyokuwa wakifanya wapiga debe wengine.
Japokuwa alishikwa kibabe lakini Winfrida akachanganyikiwa, mapigo ya moyo wake yakapiga kwa nguvu, akahisi mwili wake ukipigwa na shoti ya umeme, mguso ule ulimchanganya na kujikuta akiachia tabasamu pana.
“Unakwenda dada? Ingia! Twende dada! Kuna siti za kumwaga, utakaa na ukichoka utalala,” alisema Godwin.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kuonana na Godwin. Moyo wake ulichanganyikiwa, aliporudi nyumbani, alijilaza kitandani na kuanza kumfikiria mwanaume huyo. Alionekana kuwa mvuta bangi, aliyepigwa na maisha lakini kwa Winfrida hakujali, alimpenda, kwa jinsi alivyokuwa, kwa muonekano wake uleule, moyo wake ukamkubali kwa asilimia mia moja.
Safari za kwenda Makumbusho hazikuisha, kila siku alikuwa akielekea huko hata kama hakuwa na kitu chochote kile. Alipofika, hakupanda kwenye daladala yoyote ile, alisimama pembeni na kumwangalia Godwin jinsi alivyokuwa akiita abiria, moyo wake ulimuonea huruma lakini hakuwa na jinsi.
“Mbona unapata tabu hivi! Hutakiwi kupata tabu hata kidogo,” alisema Winfrida huku akimwangalia mwanaume huyo.
Moyo wake ukafa na kuoza, penzi likaingia moyoni mwake kwa kasi kubwa. Darasani alipokuwa akisoma, hakusoma kwa raha, aligubikwa na mawazo tele na muda mwingine alikuwa akizungumza peke yake kama kichaa.
Happiness aliligundua hilo, alijaribu kumuuliza Winfrida kilichokuwa kikiendelea lakini msichana huyo hakuwa radhi kumwambia zaidi ya kumdanganya kwamba alikuwa na matatizo ya kifamilia.
“Kweli?”
“Ndiyo Happy! Siwezi kukuficha chochote kile,” alisema Winfrida huku akimwangalia rafiki yake usoni, ili kumdanganya zaidi, akamtolea tabasamu pana.
Happiness hakuhoji sana, alimuacha Winfrida ambaye aliendelea kuteseka kila siku moyoni mwake. Safari za kwenda Makumbusho ziliendelea huku lengo lake kila siku likiwa lilelile la kumuona mwanaume huyo ambaye tayari aliingia moyoni mwake, akavuta kiti na kutulia kabisa.
Aliteseka sana, baada ya miezi miwili, hakutaka kuteseka zaidi, alichokifanya ni kuamua moyoni mwake kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima amfuate mwanaume huyo na kumwambia ukweli, jinsi alivyokuwa akimpenda na kumtesa kila siku usiku.
Siku hiyo alijipanga, alioga vizuri na kuvaa nguo maalumu, alitaka kuonekana kama malkia machoni mwa Godwin ambaye wala hakuwa na habari naye. Alipofika chuo, alisoma ingawa kichwa chake kilikuwa kikimfikiria zaidi mwanaume huyo.
Hakukuwa na siku ambayo aliona masaa yakienda taratibu kama siku hiyo. Kila wakati alikuwa akiangalia saa yake, walimu walipokuwa wakiingia, alisonya, aliona muda ukienda taratibu sana, alitamani kuondoka chuoni hapo haraka iwezekanavyo kwani moyo wake ulishindwa kuvumilia, alijiona akiingia katika ulimwengu mwingine wa mahaba.
“Hebu niambie kitu,” alisema Happiness.
“Kitu gani?”
“Una nini?”
“Sina kitu!”
“Hapana! Hebu niambie ukweli. Unapokuwa na matatizo ninajua kipenzi, umekuwa ukiniambia kila kitu kinachokusibu, miezi hii unaonekana kutokuwa sawa kabisa. Hebu niambie ukweli! Nini kinaendelea?” aliuliza Happiness huku akimwangalia Winfrida.
Msichana huyo hakuzungumza kitu, akanyamaza na kuangalia chini. Kumwambia Happiness halikuwa tatizo lolote lile lakini alianza kujifikiria ni kwa jinsi gani msichana huyo angehisi mara baada ya kumwambia kwamba alikuwa kwenye mapenzi mazito na mwanaume aliyemuona kituoni.
“Niambie!” alisema Happiness.
“Sawa. Ishu ni kwamba moyo wangu upo kwenye mapenzi mazito! Hilo tu,” alisema Winfrida huku akimwangalia Happiness ambaye alionekana kushtuka.
“Upo kwenye mapenzi mazito?”
“Ndiyo!”
“Mwanaume gani tena huyo mwenye bahati? Edmund? Shedrack? Rahman? Hebu niambie,” alisema Happiness, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, masikio yake akayatega vizuri kusikia majibu kutoka kwa Winfrida.
“Unakumbuka siku ile tuliyokwenda Makumbusho?” aliuliza Winfrida.
“Siku gani?”
“Siku ile mpaka yule kaka akaja kutuvuta?”
“Ndiyo! Nakumbuka! Yes! Nishapata jibu! Au ndiye yule mwanaume uliyekuwa umekaa naye kwenye daladala?” aliuliza Happiness.
“Hapana!”
“Kumbe yupi?”
“Yule aliyetuvuta mikono!”
“Unamaanisha yule mpiga debe?”
“Hapana! Namaanisha yule mume wangu wa baadaye,” alijibu Winfrida huku akionekana kukasirika kwani hakutegemea kama Godwin angeitwa jina la Mpiga Debe.
Happiness akabaki kimya, alishtuka, akashusha pumzi, akamwangalia shoga yake, hakummaliza. Alimwangalia vilivyo machoni kuona kama kweli alimaanisha kile alichokuwa amekizungumza au la. Kwa jinsi Winfrida alivyoonekana, alionekana kumaanisha kila kitu alichomwambia msichana huyo.
“Imekuwaje tena?” aliuliza.
“Mapenzi!”
“Sawa. Lakini kwa yule?”
“Ndiyo!”
“Hapana! Utakuwa umechanganyikiwa Winny!”
“Bila shaka nimechanganyikiwa. Tena nimechanganywa na mapenzi mazito niliyokuwa nayo kwa yule kaka,” alisema Winfrida. Hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kusimama na kuondoka.
Hakutaka kuingiliwa, aliamua kupenda kwa moyo wote, kwake, Godwin alionekana kuwa mwanaume wa ajabu, mwenye uzri wa ajabu kuliko wanaume wote katika dunia hii.
Akaondoka mpaka Makumbusho. Siku hiyo alijipanga, hakutaka kuona akiendelea kuteseka moyoni mwake. Aliamua kumwambia ukweli kwani kama kuteseka, aliteseka sana na alitaka kuwa huru.
Alipofika Makumbusho, akateremka kwenye daladala na kwenda kusimama pembeni kabisa. Alisimama huku akimwangalia Godwin aliyekuwa bize kuita abiria.
Ilipofika saa 8:16 mchana, muda ambao mwanaume yule alielekea katika kibanda cha mama ntilie kula, naye Winfrida akasimama na kumfuata mwanaume huyo.
Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida. Alipofika katika kibanda kile, akakaa kwenye benchi, wanaume wote waliokuwa mahali pale walimshangaa, iliwezekanaje msichana mrembo kama yeye akae mahali hapo?
Hakuzungumza kitu, kwa sababuu hakuwa amekaa mbali na Godwin, akayageuza macho yake kisiri na kumwangalia mwanaume huyo, kitu kilichomshtua ni baada ya kugonganisha macho na Godwin. Moyo wake ukalia paaa! Mbaya zaidi mwanaume huyo akatoa tabasamu pana. Winfrida akahisi baridi kali, mwili ukaanza kumtetemeka na kijasho chembamba kumtoka.
“Mungu nitie nguvu,” alijikuta akisema huku akiendelea kuangalia na Godwin ambaye hakuwa na taarifa yoyote kupendwa na msichana huyo.
Je, nini kiliendelea?
Fuatilia RNGM blog

No comments