Page Nav

HIDE

Breaking News:

latest

GAMBOSHI SEHEMU YA 2

GAMBOSHI SEHEMU YA 2 “Nakupenda Anitha!” “Nakupenda pia Richard, moyo wangu wote upo kwako, hakuna kitakachobalidisha pendo langu kwako, k...

GAMBOSHI SEHEMU YA 2
“Nakupenda Anitha!”
“Nakupenda pia Richard, moyo wangu wote upo kwako, hakuna kitakachobalidisha pendo langu kwako, katika shida ama raha, daima nitakuwa wako!”
“Duh! Wewe kweli mwanamuziki, hapo pote umemwaga mashairi!” Richard akatania kwa sauti ya chini chini wote wakacheka.
Ukumbi ulikuwa umegubikwa na vifijo, nderemo na vigelegele, Wimbo wa Anitha ulikuwa umewasisimua watu wote, waliokuwa wakilia tayari walikuwa wakijifuta machozi ili kusubiri hatua iliyokuwa ikifuata, kila mtu alikiri kwamba kweli Anitha alikuwa na uwezo wa kuimba na alistahili tuzo zote alizowahi kupokea.
MC, Clay aliyekuwa akiendesha shughuli hiyo aliwarudisha maharusi moja kwa moja kwenye viti vyao ambako waliendelea kuketi wakinywa vinywaji taratibu na kuongea maneno machache, hakika ilikuwa ni siku ya furaha kwa wote wawili.
Saa sita kamili MC alitangazwa kuwa muda wa bwana na bibi harusi kuondoka ukumbini kwenda kupumzika kwenye Hoteli ya Tilapia ulikuwa umewadia, Anitha na Richard wakaongozwa moja kwa moja hadi nje ya ukumbi ambako waliingia kwenye gari na msafara ukaanza safari kwenda kwenye hoteli Tilapia iliyokuwa ufukweni mwa Ziwa Victoria, huko wote wawili walishuka na wapambe pamoja na wageni waalikwa wao na kusindikizwa hadi vyumbani kwao ambako walilala mpaka asubuhi ya siku iliyofuata.
Hoteli nzima ilikuwa imejaa wageni wa Richard toka sehemu mbalimbali za Tanzania na nje waliokuwa wamekuja kuhudhuria harusi, asubuhi hiyo wakati wa kustaftahi walianza kuongea juu ya mpango wa fungate lao, ambalo Richard alipanga kusafiri hadi kwenye hoteli ya Kitalii iitwayo Kijereshi ambayo iko mwanzo wa mbuga ya Serengeti upande wa Mkoa wa Mwanza baada tu ya kuondoka kwenye mji uitwao Lamadi, hakutaka kwenda nchi za nje, yeye na wageni wote aliongozana nao walipenda kutembelea mbuga hiyo kuona wanyama. Siku nne baadaye, msafara kuelekea kwenye fungate ulianza, wakawasili na kupokelewa kwenye hoteli hiyo iliyojificha katikati kabisa ya mbuga, wote iliwavutia.
Siku hiyo hawakutoka, lakini iliyofuata Richard akiwa amevaa fulana ndogo iliyoacha mabega wazi pamoja na bukta, Anitha akiwa ndani ya suruali nyepesi ya lineni na kiblauzi cha rangi ya pinki, wote wakiwa wamevaa miwani ya rangi nyeusi sababu ya jua walipanda ndani ya gari la kifahari aina ya Hummer nyeusi, Richard alinunua gari hiyo nchini Marekani mwaka mmoja kabla na kuituma nyumbani ili awe akiitumia anapokuja likizo, hakuwepo mtu mwingine mwenye gari ya aina hiyo katika nchi nzima ya Tanzania! Taratibu walikula kiyoyozi wakiendelea kusikiliza muziki na kuzama porini wakiangalia wanyama, Anitha alikuwa ametokeza kwa juu akipiga picha kila alipoona kitu kizuri.
Kwa masaa manne walitembea huku na kule bila kuchoka, kila kitu kiliwavutia hatimaye wakaamua kuegesha chini ya mti wenye kivuli na kuanza kupigana mabusu, katika hali ambayo hawakuitegemea ghafla walishtuka mvua kubwa ikianza kunyesha, iliambatana na radi na vimbunga! Wote walishindwa kuelewa ilitokea wapi kwani hapakuwa na dalili ya mawingu.
“Hii mvua sijui imetokea wapi?” Anitha aliuliza.
“Achana nayo sisi tuendelee kula raha zetu!”
“Lakini tunahitaji kurudi hotelini, giza litaanza kuingia!”
“Hakuna shida, hapa nilipo nina bastola iliyojaa risasi!”
Walibaki hapo kwa masaa matatu, ndipo Richard akaamua kugeuza gari ili waondoke, akashangaa tairi zilipozama udongoni kumbe sehemu waliyokuwa wameegesha palikuwa na udongo mbaya wa mfinyanzi, gari ikawa imekaa ardhini! Akijiamini, Richard alicheka na kuingiza gia nyingine fupi iliyoko mbele ya ndefu, hiyo iliitwa four wheel driver, kwa ajili ya kuzungusha tairi zote ili zing’oke kwenye tope, cha kushangaza zaidi haikusaidia, gari ikazidi kutitia! Moyo ukaanza kumdunda.
“Sijui tutafanya nini?”
“Wapigie simu waje watusaidie!”
“Sawa!” aliitikia Richard lakini alipotoa simu yake hapakuwa na mtandao eneo hilo.
“Vipi?”
“Hakuna network!”
“Sasa tutafanyaje?”
“Subiri!”
“Unataka kufanya nini?”
“Acha nikaangalie chini, inawezekana kuna tatizo!”
“Richard, tuko mbugani unaweza kuliwa na wanyama?”
“Sasa tufanyaje mke wangu?” aliuliza Richard huku miungurumo ya Simba ikisikika.
“Tusubiri mpaka asubuhi!”
“Hapana, acha nijaribu kufanya kitu!” aliongea Richard na kuchukua bastola yake ikiwa imewekwa tayari na kushuka hadi chini ambako alizama uvunguni mwa gari na kugundua kulikuwa na mzizi ulioshikilia tairi, kwa furaha akatoka uvunguni na kuzunguka hadi nyuma ambako alichukua shoka na kurudi kuukata, alipomaliza aliwasha gari na kuigiza gia fupi, mara moja gari ikang’oka na safari ikaanza.
“Hureeee!” Anitha alishangilia.
Usiku mzima walisafiri bila kufika hotelini, kulipokucha walishangaa kujikuta bado wako pale pale! Bila kusogea hata hatua moja, wakaangaliana kwa mshangao, walishindwa kuelewa ni jambo gani lilikuwa limetokea, walikuwa wameota ndoto? Walijiuliza swali hilo na kugundua haikuwa kweli, maana shimo walilokuwa wamezama lilikuwepo nyuma yao.
“Nini kimetokea?”
“hata mimi sielewi mke wangu, nimeendesha gari usiku mzima nashangaa kujikuta bado tuko hapa?”
“Mh! Hebu washa tena tujaribu” Anitha alishauri akiwa amejawa hofu, halikuwa jambo la kawaida hata kidogo, hakuna alichokifikiria akili mwake zaidi ya nguvu za giza.
Katika hali ya kushangaza kabisa, gari likaruka kama limeachiwa na watu, safari yao ikaanza na kusafiri kwa karibu masaa matatu bila kuongea chochote, mioyo yao ikiwa imejawa na hofu. Kwenye kona kali iliyokuwa mbele yao, Richard hakuwa mwangalifu, akashangaa kukutana uso kwa uso na lori kubwa aina ya Benzi ambalo liligonga gari lao na kupanda hadi juu, wakagandamizwa.
“Richard nisaidie nimebanwa!”
“Hata mimi nimebanwa!”
Je nini kitaendelea?
Je ni kitu gani kimetokea?

Fuatilia RNGM blog

No comments