Page Nav

HIDE

Breaking News:

latest

HARMONIZE AWEKA REKODI KUBWA AFRIKA

DAR ES SALAAM: Mambo yamemyookea! Ndiyo lugha rahisi unayoweza kutumia kuwasilisha mafanikio ya haraka anayoendelea kuyapata, staa wa Bong...


DAR ES SALAAM: Mambo yamemyookea! Ndiyo lugha rahisi unayoweza kutumia kuwasilisha mafanikio ya haraka anayoendelea kuyapata, staa wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul Kahali ‘Harmonize’.

KISHINDO CHA KWANGARU REMIX

Habari njema zaidi kwake kwa kipindi hiki ni kwamba, ameiandika rekodi ya aina yake Afrika kufuatia kishindo cha wimbo wake wa Kwangaru Remix kusikilizwa katika mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
loading...

Iko hivi, Harmonize alijiwekea rekodi hiyo kwa wimbo wake huo kupigwa katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Posta jijini Dar, eneo ambalo marais 11 na mawaziri wakuu wa nchi nyingine nne zinazounda Umoja wa Sadc na ujumbe wao (viongozi wengine waandamizi wa nchi hizo) walikutana na kufanya mkutano wao wa kihistoria.


REKODI

Rekodi za hapa nchini zinaonesha kuwa, hakuna msanii wa Bongo Fleva ambaye wimbo wake ulipigwa kwenye eneo moja ambalo limewakutanisha marais wa mataifa 11, mawaziri wakuu na viongozi wengine wakuu wa serikali katika mkutano wa Sadc.

Wapo wasanii kadhaa akiwemo Harmonize walioweza kupenya nchi mbalimbali duniani, lakini hakuna msanii wa Tanzania ambaye amepata nafasi ya kusikilizwa na viongozi wakuu wa nchi 16 kwa wakati mmoja.

Harmonize anakuwa msanii wa kwanza kutazamwa, kufuatiliwa, kuripotiwa na kutazamwa na mataifa 16 duniani kwa wakati mmoja. Ikumbukwe, wakati tukio hilo likitokea, waandishi wa habari wa nchi hizo walikuwepo ukumbini hapo wakichukua tukio hilo na kuhabarisha umma kupitia vituo vya nchi zao.

FULL KUWAPAGAWISHA VIONGOZI

Mbali na kuweka rekodi hiyo, kitendo cha wimbo huo wenye ujumbe wa maendeleo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kupigwa ukumbini humo, viongozi mbalimbali walilipuka kwa shangwe ambapo baadhi yao waliinuka na kucheza pamoja huku wakiangalia video yake katika ‘skrini’ kubwa.

Risasi Mchanganyiko lililokuwemo ukumbini humo, lilishuhudia waandishi wa habari ambao waliambatana na viongozi wa nchi zao ambao waliurekodi na kuweka wazi kuwa unakwenda kurushwa kwenye nchi zao katika vipindi maalum.

KUTIKISA NCHI ZA SADC

Walisema, Harmonize pamoja na baadhi ya wasanii wengine wa ngoma za asili waliopata nafasi ya kupafomu kwenye mkutano huo, wanakwenda kuwa gumzo kwenye vyombo mbalimbali vya habari vya nchi 16 zinazounda Sadc.

“Hii ni zaidi ya promosheni kwa huyu msanii, wimbo wake umebeba dhana ya uwajibikaji kama taifa kupitia maendeleo makubwa ambayo Tanzania imeyapiga. Mfano ununuzi wa ndege, miradi mikubwa ya umeme, barabara na kadhalika,” alisema mmoja wa waandishi wa habari wa Zimbambwe ambaye hakupenda kutaja jina lake.

MITANDAONI KWACHAFUKA

Kabla hata ya vipindi hivyo maalum havijarushwa kwenye runinga mbalimbali hususan zile za taifa, tayari kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii liliibuka gumzo kubwa tangu wikiendi iliyopita.

Video ya Harmonize ambayo inaonesha miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa nchini ndiyo iliyokuwa ‘ikitrendi’ kwenye mitandao ya nchi hizo ambazo ni Angola, Botswana, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe.

AKUTANA NA JK

Kama ilivyoandikwa kwenye maandiko matakatifu kwamba mwenye nacho ataongezewa, mbali na shavu hilo alilolipata, jioni ya siku hiyohiyo Jumapili aliyojiandikia historia yake katika mkutano wa Sadc, Harmonize alialikwa kwenye dhifa ya kitaifa Ikulu na kupata bahati nyingine ya kukutana na viongozi mbalimbali wastaafu walioalikwa akiwemo Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete.

Alipokutana na Dk. Kikwete, Harmonize aliweka wazi kuwa amefurahi kukutana naye na kwamba anamuahidi makubwa katika gemu ya Bongo Fleva.


HUYU HAPA HARMONIZE

“Jana nilipata nafasi ya kujumuika katika dhifa ya taifa iliyoandaliwa na rais wetu kipenzi Dk. John Pombe Magufuli State House jijini Dar es Salaam, naamini nilikuwa pale kuwakilisha vijana wengi walio mtaani na wenye ndoto.

“Hakika ilikuwa bahati kwangu kukutana na viongozi wa ngazi za juu kabisa kila niliyekutana naye pale ndani alinipongeza sana na kuniambia wanajivunia uwepo wangu katika hili taifa tukufu, ilinipa moyo na somo la kwamba kupitia kipaji chako au kazi yako hiyo hiyo ifanye kwa bidi utatimiza kila aina ya ndoto yako na kupewa kila aina ya heshima. Kijana mwenzangu chukua hiyo!

“Lakini mwishoni kabisa nikakutana na swahiba Former President Dr Kakaya Mrisho Kikwete, tulifurahi sana akaniambia wewe sasa hivi sio msanii tena wewe ni mwanamuziki ni wakati wa kuifanya Tanzania iendele kuwa proud na wewe.

Watanzania wote wanakupenda na wanakusupport go go go…..! Nami nikamwambia sitoweza kuwaangusha na sitoweza kuku-disappoint yaani subiri tu uone hili movie linavyoenda! Akacheka sana mwisho akaniambia mimi nakutakia kila la heri! Love you dady.”

KAULI YA JK YAMTIKISA MONDI

Baada ya kuweka picha yake na Kikwete mitandaoni, wadau mbalimbali walitoa maoni yao ambapo wengi wao walisema wanauona ufalme wa mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ ukiwa shakani kutokana na kauli aliyopewa na Kikwete kwamba yeye ni mwanamuziki anayetegemewa.

“Kauli ya JK inamuwashia taa nyekundu Mondi, awe makini sana wewe angalia dogo (Harmonize) anavyowateka viongozi wa nchi, wimbo wake wa Kwangwaru alipouachia, viongozi kibao wa Serikali waliuposti mitandaoni, angalia mialiko mikubwa ya kitaifa kama hii anaitwa Harmonize wakati tulitegemea shavu kama hili lilikuwa la kwake,” alichangia mdau mtandaoni aliyejiita Kinesi.

Mwingine aliyejiita Banne P, aliandika: “Lakini lazima athibitishe uwezo wake kwa kutovimba kichwa. Ujue mafanikio kama haya yakimvimbisha kichwa, anaweza kuangukia pua. Akaze, asiwaangushe Watanzania. Namuona ni mkali, ila asimdharau Diamond, ndiye aliyemshika mkono.”

No comments